Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Adam Malima ametoa rai kwa wananchi wanaozunguka Mradi wa Ujenzi wa daraja la JP Magufuli (Kigongo-Busisi) linalotekelezwa kwa Shilingi Bilioni 700 kuacha tabia ya wizi na udokozi wa vifaa kwenye mradi huo ili likamilike kwa wakati na kuwahudumia wananchi.
Amesema hayo leo Disemba 02, 2022 Ofisini kwake wakati alipotembelewa na Uongozi wa kampuni ya Mkandarasi anayetekeleza ujenzi wa Daraja China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) hilo lenye urefu wa KM 3.2 na kuzungumza na Waandishi wa Habari.
Aidha, Mhe. Malima amebainisha kuwa kutakua na ucheleweshaji wa kukamilika kwa daraja hilo kwa miezi 8 hadi Novemba 2024 badala ya februari 2024 iliyopo kwenye Mkataba kutokana na Vifaa vya ujenzi wa mradi huo kupatikana kutoka nje ya nchi ambako pia wamekubwa na janga la Ugonjwa wa Uviko 19.
"Tukipata ucheleweshaji kutokana na Ugonjwa wa Covid 19 inawezekana lakini sio kwa udokozi huo ambao ni sawa na uhujumu uchumi, watafute biashara ingine ya nondo na vyuma lakini sio kwenye Miradi ya kitaifa maana tutawatolea mfano waone kisirani chetu maana hatuko tayari kurudishwa nyuma na watu hao." Mhe. Malima.
Ameongeza kuwa katika utekelezaji wa Ujenzi wa mradi huo Serikali ya Mkoa imejidhatiti kuweka hali ya Usalama ili kuhakikisha Mkandarasi anafanya kazi usiku na mchana ili kufanikisha ukamilishaji kwa amani, na kwamba kuanzia anayeiba, aliyepakia kwenye gari, atakayenunua na atakayejengea vyuma hivyo wote watakua hatiani.
"Hapa katikati palitokea sintofahamu ya udokozi wa vifaa pale kwenye mradi kama vyuma, nondo na vitu vingine nasi kama kamati ya usalama ya Mkoa tumejidhatiti kuhakikisha haliendelei suala hilo." Amesisitiza Malima.
Vilevile, ametoa rai kwa wananchi kuacha usumbufu kwa mafundi wanaojenga daraja hilo kwa kuwaingilia kwa kutumia daraja la Ujenzi ambalo sio lengo lake bali watakaokuwa na dharula nje ya Magari ya wagonjwa na Usalama watapaswa kupata kibali maalum kutoka kwa katibu Tawala Mkoa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.