Wanachama na wadau wa Chama cha Wanasayansi wa Maabara za Afya Tanzania (MeLSAT) Mkoa wa Mwanza wametakiwa kushiriki kikamilifu shughuli mbali mbali za chama kama njia ya kuendelea kudumisha huduma kwa wananchi
Wito huo umetolewa leo Aprili 25 2023 na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Bw. Balandya Elikana wakati akifungua Maadhimisho ya Wiki ya Wataalam wa Maabara Mkoa wa Mwanza katika viwanja vya Furahisha Wilaya ya Ilemela.
Bw. Balandya ameongeza kuwa wadau na wataalam wa maabara watumie maadhimisho hayo kama njia ya kuboresha huduma katika Mkoa wa Mwanza na Tanzania kwa ujumla.
"Nitoe wito kwa wataalam wote wa Maabara Mkoa wa Mwanza kuwa wanachama hai wa Chama cha Wanasayansi wa Maabara za Afya Tanzania (MeSALT) na kushiriki katika shughuli mbali mbali za chama pia Waajiri mtoe ruhusa kwa Wataalam wa Maabara kushiriki shughuli za chama bila kuathiri utoaji huduma kwa wananchi," Amesema Mtendaji huyo wa Mkoa
Aidha Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dkt. Thomas Rutachunzibwa amesema Mkoa wa Mwanza unaendelea kuhakikisha kuwa huduma za afya zinazotolewa zinakuwa bora kwa kusimamia ubora wa huduma za maabara za Serikali na za watu binafsi.
"Mkoa wa Mwanza kupitia timu ya usimamizi wa huduma za afya tunaendelea kusimamia na kuhakikisha kuwa huduma zote za afya zinazotolewa zinakuwa bora kwa kusimamia ubora wa huduma za maabara za Serikali na watu binafsi," amesema Rutachunzibwa
Pia Mwenyekiti wa Chama cha Wanasayansi wa Maabara za Afya Tanzania (MeSALT) Bertrand Msemwa amesema anaiomba serikali kuendelea kuajiri wataalam wa Maabara ili waweze kufanya kazi katika kiwango ambacho kinatakiwa na huduma ziweze kutolewa nzuri.
Naye Katibu wa Chama cha Wanasayansi wa Maabara za Afya Tanzania (MeLSAT) Mkoa wa Mwanza Bw. Yusuphu Mkama amesema wananchi wa Mkoa wa Mwanza wafike sehemu maadhimisho yanapofanyika ili waweze kupatiwa huduma za vipimo bure.
"Niwaombe wananchi wa Mkoa wa Mwanza muweze kufika mahali hapa ambapo maadhimisho yanafanyika muweze kupatiwa huduma na kujua afya zenu kwakuwa huduma za vipimo ni bure,"amesisitiza Mkama
Maadhimisho hayo yamefanyika Ki- Mkoa kwa mara ya 2 ikiwa ni maadhimisho ya 12 tangu kuanzishwa ambayo yanafanyika kwa muda wa wiki moja kuanzia Aprili 24 hadi Aprili 28 2023.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.