*Watumishi wa Umma Mwanza wakumbushwa kutambua wajibu wao*
Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma Mhe.Jaji mstaafu Hamissa Kalombola amewataka watumishi wa Umma kufanya kazi huku wakitambua wajibu na stahiki zao ili kuepusha migogoro pale linapokuja suala la kuchukuliana hatua za kinidhamu.
Akifungua leo Mkutano wa kikao kazi kwenye ukumbi wa Rock City Mall kilichowahusisha watumishi wa Umma, Mwenyekiti Mhe.Amisa amesema Tume yake imekuwa ikipokea mashauri mengi yanayochangiwa na watumishi kutofahamu au kuzembea kizingatia miongozo iliyopo ya Utumishi wa Umma.
Ameongeza kuwa Tume yake inachukua hatua ya kutembelea watumishi mikoani lengo likiwa kupeana elimu na kukumbushana kufanya kazi kwa maadili ili kila mmoja atimize majukumu yake na kufikia malengo.
"Maafisa Utumishi mliopo hapa nyie mna wajibu wa kuwafahamu vizuri watumishi wenu na hata anapotokea mtumishi amebadilika ghafla tabia kama utoro,muite msikilize nini tatizo kabla hujamchukulia hatua." Mhe. Hamissa Kalombola
Naye Kamishna wa Tume hiyo, Mhe.Balozi Adadi Rajabu amebainisha Tume yao ina malengo makuu matatu ambayo ni Ushauri kwa Mhe.Rais, ulekevu na kusimamia utoaji wa haki, lengo kwa ujumla watumishi wote wa Umma nchini wafanye kazi katika mazingira sahihi na rafiki.
"Mhe Rais wetu siku zote anapenda kuwaona watumishi wa Umma wakifurahia mazingira yao ya kazi mfano mzuri tumemsikia akizungumza wakati wa Mei Mosi Kitaifa mwaka huu Mkoani Morogoro, hivyo sisi watumishi wajibu wetu ni kurudisha asante kwa kufanya kazi kwa uadilifu ili kulijenga Taifa," Amesema Mhe.Balozi Adadi Rajabu.
Awali alimkaribisha Mwenyekiti wa Tume hiyo,Ndg.Daniel Machunda Katibu Tawala Msaidizi,Utawala na Rasilimali watu akimwakilisha Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza,amesema kikao kazi hicho kwa watumishi wa Umma kitakuja na matokeo chanya ya uwajibikaji makazini huku kila mmoja akiheshimu Sheria zilizopo.
"Tunajitahidi kufanya kazi kwa kizingatia Sheria,kanuni na taratibu zilizopo na wakati mwingine kukumbushana miongozo inavyotaka,"Machunda.
Kikao kazi hicho kimewashirikisha watumishi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa,ofisi ya Mkuu wa Wilaya Nyamagana,watumishi wa Jiji la Mwanza na Manispaa ya Ilemela.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.