Watumishi wa umma wametakiwa kufanya kazi kwa utii, kuzingatia sheria,kanuni na miongonzo ya utumishi katika utoaji huduma bora kwa wananchi pamoja na kutumia taaluma zao kuleta mabadiliko chanya.
Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora Dkt.Mary Mwanjelwa wakati akizungumza kwenye mkutano na watendaji wa taasisi za umma Mkoani Mwanza alisema,wananchi wote wanahitaji huduma mbalimbali kutoka Serikalini ambao wanatoa huduma hizo ni watumishi wa umma,hivyo katika kutekeleza hilo wanapaswa kufanya kazi kwa utii na kuzingatia sheria na siyo kwa mazoea.
"Mtumishi wa umma anapaswa kufanya kazi mahali popote kwa utii na wajibu wake ni kutoa huduma bora kwa wananchi pamoja na kuwa mbunifu,mvumilivu na mzalendo licha ya kuwa changamoto zipo, anatakiwa kutumia utaalamu na weledi wake kuleta mabadiliko chanya mfano eneo ambalo mapato yake ni kidogo kupitia yeye yaongezeke palipo na utovu wa nidhamu na maadili yawepo," alisema Dkt.Mwanjelwa.
Pia alisema,kitendo cha mamlaka za nidhamu kutozingatia sheria, kanuni na taratibu wakati wa kushughulikia masuala ya nidhamu kinaisababishia Serikali hasara pale inapolazimika kuwalipa watumishi mishahara ambayo hawakifanyia kazi ikiwa pamoja na kuanzishwa upya kwa mashauri hayo na watumishi kurejeshwa kazini.
"Kutokana na kitendo hicho nawaagiza watendaji wakuu wa taasisi zote za umma kuhakikusha kwamba mashauri ya nidhamu yanaendeshwa kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma,hivyo wale ambao watakiuka tume ya utumishi wa umma izijulishe mamlaka zao za nidhamu stahiki zichukuliwe dhidi yao mara moja," alisema.
Aidha alitumia fursa hiyo,kuwaagiza kila mwajiri kuhakikisha watumishi wake wanapata elimu kuhusu dhana nzima ya OPRAS ili waweze kuielewa na kutekeleza kikamilifu,wanajaza kikamilifu na kufanya tathmini ya utendaji kazi wao kwa ajili ya kuhakikisha malengo yaliyowekwa na taasisi yanafanikiwa.
"Suala la ujazaji OPRAS ni takwa la kisheria kama inavyobainishwa na kifungu cha 6 cha sheria ya utumishi wa umma sura ya 298,hata hivyo takwimu zinaonesha kuwa suala hilo bado halipewi umuhimu unaostahili,taarifa za kaguzi mbalimbali zinazofanywa na tume kuhusu usimamizi na uendeshaji wa masuala ya rasilimali watu zinaonesha kuwa OPRAS bado ni changamoto kubwa kiutekelezaji hivyo waajiri wanapaswa kulisimamia jambo hilo," alisema.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Christopher Kadio alisema, manufaa ya mkutano huo ni kufumbuliwa macho kwa kuwajengea uelewa mzuri wa sheria ya utumishi wa umma na kugundua miongoni mwao wapo watu ambao watawatumia katika kuboresha sekta hiyo pamoja na kupata fursa ya kutambua matatizo yao huku akiwahimiza watendaji na watumishi kujitoa katika kuhudumia wananchi kwa maendeleo ya taifa.
Naye Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma Balozi Mstaafu John Haule alitoa wito kwa watendaji wa taasisi za umma kuwapa fursa na kuwatumi maofisa utumishi na wanasheria kwani wanajua tafsiri za sheria hiyo ya utumishi huku mamlaka zitakazokuwa tayari kugharamia watumishi wake timu ya tume hiyo itakuja kuwaelimisha namna ya kutekeleza sheria,kanuni na taratibu za utumishi wa umma.
Aidha Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Cornel Magembe alisema,tume ya utumishi wa umma ifungue milango wazi watu wakasome wasilazimishwe kusomea kitu alichonacho mwanzo mfano walimu wapewe fursa ya kusomea vitu vingine ili wasaifie jamii katika nyanja nyingine huku Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Dkt.Severine Laika aliomba mafunzo ya OPRAS yaongezwe kwani ni nzuri.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.