WAZIRI DKT. NDUMBARO AWATAKA WALIONG'ARA UMISSETA NA UMITASHUMTA WAITWE TIMU YA TAIFA MASHINDANO YA FEASSSA
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amemtaka Mkurugenzi Msaidizi wa michezo Dkt. Ado Komba kuhakikisha anawaingiza wachezaji hodari na wenye vipaji kutoka Mkoa wa Mwanza waliofanya vizuri katika mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA 2024 yaliyofanyika Mkaoni Tabora kuingizwa kushiriki katika mashindano ya shule za nchi za Afrika Mashariki (FEASSSA) yatakayofanyika nchini Uganda.
Wanamichezo hao ni Neema Mkula ambaye alikuwa mfungaji bora mpira wa pete mashindano ya UMITASHUMTA akiwa na jumla ya magoli 360, Magreth Manawa mfungaji bora mpira wa kikapu UMISSETA ana jumla ya vikapu 110 pamoja na Agnes John mfungaji bora mpira wa pete ana jumla ya magoli 290.
Mhe. Dkt. Ndumbaro ametoa agizo hilo leo Julai 01 2024, alipokuwa akizungumza wakati wa kukabidhi jumla ya makombe 31 kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda (12 kwa UMITASHUMTA na 09 kwa UMISSETA), Aidha Mkoa wa Mwanza ulifanikiwa kuwa mshindi wa jumla kwanza katika mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA Kitaifa 2024.
Waziri huyo wa Michezo amesema wanafunzi hao wamefanya vizuri na kwa kuwa michezo hiyo imechezwa hadharani na ulikuwa mchezo wa wazi hivyo wamekidhi kuchaguliwa kushiriki kwenye mashindano ya Shule za Nchi za Afrika Mashariki (FEASSSA) yatakayofanyika nchini Uganda.
Waziri Ndumbaro amesema michezo ni ajira na michezo ni uchumi, hivyo ukiona una kipaji au una umahiri wa mchezo wowote ule basi hakikisha unanakiendeleza kipaji hicho kwani zama zimebadilika sana, unaweza kuajiriwa kupitia kipaji hicho.
"Hapa nchini kuna wachezaji wanalipwa mil. 50 kwa mwezi hata mimi Waziri Ndumbaro na RC hapa hatufikii hata robo hivyo ukiona una kipaji kiendeleze maana ni ajira".Waziri Ndumbaro
Amesema UMITASHUMTA na UMISSETA ndio chimbuko la mafaniko kwa vijana wengi watakaokuja kuwa wachezaji wakubwa na ambao pia watakwenda kushiriki katika michuano mbalimbali kimataifa,hivyo hatuna budi kuviachilia vipaji vyetu vikapotea wakati huo tayari ni mtaji.
Aidha Dkt. Ndumbaro amesema Tanzania inatarajia kuandaa mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, hivyo amewataka wale wote wanaofanya skauti ya wanamichezo kuhakikisha wanawaibua wachezaji mahiri na hodari ili waweze kushiriki katika Timu ya Taifa.
"Hatuwez kuvuna bila kupanda, lazima tupande ndipo tuvune na sasa ndio wakati mzuri wa kuwaandaa vijana wetu ili ifikapp 2027 tuwe na timu nzuri ya mashindano",Waziri Ndumbaro
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amewawapongeza wanamichezo wote kutoka Mwanza kwa heshima kubwa waliouletea Mkoa huo, kwani wameuheshimisha kwa kuleta makombe mengi.
Aidha Mhe. Mtanda ametoa maagizo kwa Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Bw. Balandya Elikana kupitia kwa Afisa Elimu na Utamaduni kwa wale wanafunzi wote 18 waliofanya vizuri kuhakikisha wanapata zawadi ili iwawahamasishe hata wengine.
Agizo hilo tayari limetekelezwa na wale wote waliofanya vizuri katika mashindano hayo wamepatiwa zawadi ya fedha taslimu kiasi cha Tsh. Laki moja kwa washindi, wachezaji bora, hodari na waliochaguliwa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.