Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI)Mhe. Suleiman Jaffo amewataka watendaji kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato wa Manispaa ya Ilemela, ambayo ni miongoni mwa manispaa zenye vyanzo vingi vya mapato.
Jaffo ameyasema hayo wakati alipokuwa akizungumza na watendaji na wafanyakazi wa Manispaa ya Ilemela ambapo alipata fursa ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya afya na barabara ambayo inatekelezwa chini ya Wizara yake, wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja katika manispaa hiyo.
Kwenye mkutano wake na watumishi wa manispaa hiyo, Jaffo aliwasimamisha Mchumi wa Manispaa hiyo Amosy Zephania na Mtunza Hazina wa Manispaa hiyo Jamea Dalasia ili kueleza mikakati waliyoweka kuhakikisha nakusanya mapato na kufikia malengo waliyoweka kama Manispaa.
“ Kwenye suala la ukusanyaji wa mapato, nilichokigundua kwa baadhi ya maeneo mengi ni uzembe wa baadhi ya watumishi na msikubali mtu mmoja akawaharibia kazi”, alisema Mhe.Jaffo.
Alimtaka Mkurugenzi Mtendaji wa manispaa ya Ilemela John Wanga kuwa mkali na kuhakikisha kuwa anawachukulia hatua kali baadhi ya watumishi walio chini yake wenye malengo ya kukwamisha juhudi za ukusanyaji wa mapato.
“ Kamati ya fedha na mipango simamieni vizuri ukusanyaji wa mapato ya manispaa yenu, makosa ya mtu mmoja yanaweza kusababisha manispaa yenu kusemwa vibaya,"alisema Mhe.Jaffo.
“ Unapoona manispaa yenu inasemwa vibaya, maana yake unaharibu jina la Mkuu wa Mkoa, Mkuu wenu wa wilaya na kamati nzima ya fedha,tubadilike na tuache kufanya kazi kwa mazoea."
Katika hatua nyingine Jaffo alimpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa manispaa hiyo John Wanga kwa kufanya maboresho ya ukusanyaji wa mapato kwenye Soko la Kimataifa la Mwaloni ambapo makusanyo yamepanda kutoka Sh milioni 34 hadi kufikia Sh. milioni 54 katika kipindi cha kuanzia Oktoba mosi hadi Oktoba 21 mwaka huu.
Kwa mujibu wa Wanga, ufanisi huo wa ukusanyaji wa mapato katika soko hilo, umetokana na manispaa hiyo kununua mizani ya kisasa ya kupimia mazao ya samaki, hali ambayo imeongeza mapato hayo maradufu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.