WAZIRI MKUU AHIMIZA USIMAMIZI UKAMILISHAJI MRADI WA MAJI KISESA
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa (Mb) amewataka Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) kuendelea kusimamia kwa karibu ujenzi wa tanki la maji la lita Milioni 5 ili wananchi wanaosubiri huduma hiyo wapate kwa wakati.
Mhe. Waziri Mkuu ametoa agizo hilo mapema leo tarehe 21 Desemba, 2024 kwenye Kijiji cha Bujora - Kisesa wilayani Magu alipofika kukagua mradi wa ujenzi wa tanki la kuhifadhia maji Safi (Lita Milioni 5) linalogharimu zaidi ya Tshs. Bilioni 3.5.
Mhe. Majaliwa amesema ni lazima asilimia 7 zilizobaki kukamilisha ujenzi huo ni muhimu ili kuruhusu maji ya ziwa Victoria kutoka chanzo cha Butimba kufika hapo na kusambazwa kwenye maeneo ya Bujora, Bukandwa, Kisesa na maeneo ya jirani ya Ilemela kwa wananchi elfu 75.
Aidha, amewaagiza wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira vijijini (RUWASA) kutumia vema mtambo wa kuchimba visima vya maji uliotolewa na Serikali kufanya hivyo kwa haraka kila inapohitajika ili wananchi wote vijijini wapate maji safi na salama.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ametumia wasaa huo kuwapongeza na kuwashukuru Wizara ya Maji pamoja na MWAUWASA kwa kuchapa kazi na kuhakikisha wanamtua mama ndoo kichwani kwa kutekeleza miradi ya maji kila kona ya Mkoa huo.
Akitoa taarifa ya mradi, Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA Bi. Nelly Msuya amesema benki ya Ulaya na Shirika la Maendeleo la Ufaransa kwa kushirikiana na Serikali wanatekeleza mradi huo ambao umeshatekelezwa kwa 93% hadi sasa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.