WAZIRI MKUU AZINDUA WIKI YA VIJANA KITAIFA 2024
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) leo Oktoba 11, 2024 amezindua maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa mwaka 2024 yanayofanyika katika viwanja vya Furahisha Wilaya Ilemela, Mkoani Mwanza.
Akizungumza na Vijana waliojitokeza katika viwanja hivyo Mhe. Majaliwa amewataka vijana wa Kitanzania kutumia fursa za maendeleo ya kidigitali kama njia ya kujitengenezea fursa za ajira na kuacha kutumia mitandao ya kijamii kwa mambo yasiyofaa.
Kadhalika Mhe. Majaliwa amewataka vijana kufichua na kuziainisha taasisi zenye nia ovu ya kuharibu na kuvunja mila na desturi za Kitanzania, pamoja na taasisi hizo binafsi kujitambulisha na kutoa malengo ya Taasisi.
"Vijana wa Kitanzania mkipata taasisi ya namna hii toeni taarifa ili tushughulike nazo hatuwezi kuruhusu taasisi inakuja inafundisha jambo ambalo hata kwenye mila tamaduni za Taifa lako hazipo huyo anataka kuja kubomoa Taifa letu". Amesema Wazuri Mkuu Majaliwa.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu Mhe. Ridhiwani Kikwete (Mb) amewataka vijana kutumia mifumo iliyosahihi ili waweze kufikia malengo makubwa waliyonayo na kukabiliana na changamoto ya ajira.
Akizungumza wakati akitoa salamu za Mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ameishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu kwa kuuchagua Mkoa wa Mwanza kuwa ndiyo mwenyeji wa wiki ya Vijana Kitaifa.
Maadhimisho hayo yanaratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu pamoja na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar.
Kaulimbiu ya Maadhimisho hayo ni “Vijana na Matumizi ya Fursa za Kidijitali kwa Maendeleo Endelevu,”.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.