Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (MB) anatarajiwa kuwasili Mkoani Mwanza Jumanne Machi 14, 2023 kwa ajili ya Ufunguzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama barabarani Kitaifa yatakayofanyika kwenye Viwanja vya Furahisha.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Adam Kighoma Malima wakati wa Mkutano na Waandishi wa Habari uliofanyika kwenye Ukumbi wa Ofisi ya Mkoa mapema leo Jumatatu Machi 13, 2023 ambapo amesema Mhe. Waziri Mkuu atakua Mgeni Rasmi kwenye Ufunguzi wa Juma hilo ambalo litaadhimishwa katika Mikoa yote nchini.
Mhe. Malima ametumia wasaa huo kuwakaribisha wananchi wa Mwanza na Mikoa ya jirani kujitokeza kwa wingi kandokando ya barabara ya Uwanja wa ndege na kwenye viwanja vya Furahisha vilivyopo wilaya ya Ilemela ili pamoja na kumlaki na kumpokea Kiongozi huyo wapate Elimu ya Sheria, Kanuni na Taratibu za Usalama barabarani.
Ameongeza kuwa, katika Mkoa wa Mwanza takwimu za ajali kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita (Januari-Disemba 2022) zimeripoti jumla ya ajali kubwa 81, zilizosababisha vifo vya watu 71 na kujeruhi watu 96. Aidha, kwa upande wa Pikipiki zimetokea ajali kubwa 30 zilizosababisha vifo vya watu 25 na kujeruhi 26.
"Mwelekeo wa takwimu hizo sio mzuri kabisa, niwatake watumiaji wote wa Barabara katika Mkoa wa Mwanza kuzingatia Sheria na kanuni za Usalama barabarani. Vitendo vinavyoongoza sana katika kusababisha ajali hizi pamoja na Mwendokasi, ubovu wa vyombo vya Moto, Ulevi, Kulipita gari mbele bila kuchukua tahadhari, ujazaji wa abiria na mizigo uliopitiliza na kuegesha magari yaliyoharibika barabarani." Mhe. Malima.
Vilevile ameongeza kuwa Mkoa wa Mwanza una kaulimbiu ya kudumu kuhusu Usalama barabarani isemayo (Karibu Mkoa wa Mwanza, tafadhali zingatia sheria na kanuni za usalama barabaran, Epuka adhabu kali)
na akatoa wito kwa watumiaji wa vyombo vya moto kuchukua tahadhari ili kuepusha ajali.
Mhe. Malima amebainisha kuwa Maadhimisho hayo ya Kitaifa mwaka huu yanakwenda sambamba na Kauli mbiu isemayo 'Tanzania bila Ajali inawezekana, Timiza wajibu wako' na kwamba kauli mbiu hiyo inasisitiza kuwa kila mtumiaji wa Barabara akitimiza wajibu wake kutapelekea kupungua kwa ajali za Barabarani na hatimaye kuimarika kwa Usalama barabarani.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Usalama barabarani Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Ramadhani Ng'anzi ametoa wito kwa wamiliki wa vyombo vya moto kufika katika vituo vya polisi vilivyotengwa kwa ajili ya ukaguzi wa vyombo vyao na baada ya ukaguzi watapata cheti maalumu cha kufuzu kutumia barabara na kwamba Serikali imejipanga kuona kwamba katika matumizi ya barabara kitu cha kwanza kinachozingatiwa ni usalama.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.