Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa Oktoba 17, 2022 amefanya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa meli ya Mv Mwanza Hapa Kazi Tu inayojengwa katika bandari ya Mwanza Kusini Wilaya ya Nyamagana Mkoani Mwanza na kuridhishwa na hatua ya ujenzi huo ambao umefikia asilimia 73.
Akizungumza na wananachi pamoja na viongozi wa mkoa wa Mwanza baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa meli hiyo Mhe. Majaliwa amesema amefurahishwa na mwenendo wa kazi unaoendelea na kwamba kampuni ambayo serikali ilingia nayo mkataba wa ujenzi wa meli hiyo ya GAS Entec ya Korea Kusini ipo, wafanyakazi wote wapo na watanzania waliokuwa wamepunguzwa wapo.
Ikumbukwe kamba Mei 7, 2022 Waziri Mkuu Mhe. Majaliwa akiwa Mkoani Mwanza kwa ziara ya siku moja ya kikazi alikagua ujenzi wa meli hiyo na kutoridhishwa kabisa na maendeleo yake ambayo ilikuwa imefikia asilimia 65 huku mkandarasini wa kampuni ya GAS Entec ya Korea Kusini akiwa ameuza hisa zake bila kuitaarifu serikali.
Pia serikali ilikuwa imeishamlipa mkandarasi asilimia 80 ya gharama za ujenzi wa meli hiyo lakini kampuni aliyoiuzia hisa zake ilikataa kutambua ujenzi wa meli kwa madai kwamba swala hilo liko nje ya mauziano, vilevile alikuwa amepunguza wafanyakazi kutoka 118 hadi 22.
Dosari hizo zilimfanya Mhe, Majaliwa kumuagiza Afisa Uhamiaji wa Mkoa wa Mwannza akamate pasi za kusafiria za wataalamu wa Kampuni hiyo ya GAS Entec hadi wakamilishe kazi yao.
Amesema asilimia 73 zilizofikiwa ni mwenendo mzuri na mhandisi mtanzania anayesimamia mradi huo amemhakikishia kwamba dosari zote zilizokuwepo awali hazipo sasa, wanachapa kazi na kwamba mafanikio hayo yametokana na maamuzi ambayo serikali ilichukua ya kuwanyang’anya pasi za kusafiria.
“Najua kuna Watanzania walikasirika ooo wawekezaji mmewanyang’anya hati zao za kusafiria mlitaka watoroke watuachie mradi mkubwa hivi halafu ningekuwa mgeni wa nani ilitulazimu kakaa chini na nchi yao kupitia Balozi wao tukaelezana tukakubaliana kwanza kampuni iliyouza hisa zake ambayo tuliingia nayo mkataba isiondoke, yenyewe ndiyo ijenga hadi ikamilishe ujenzi wa meli yetu na wafanyakazi wote kutoka kwao walioondoka warudishwe nchini, waje waendelee na kazi yao pia wafanyakazi wa Tanzania 112 waliofukuzwa kazi warudishwe kazini na kazi ikamilike,”ameeleza
Mhe. Majaliwa amesema baada ya makubaliano mkandarasi huyo aliahidi kumaliza kazi ya ujenzi wa meli Mwezi wa 11 na itabaki kazi ndogo hivyo ameagiza muda huo ukifika iingizwe ndani ya maji kwa ajili ya kukamilisha shughuli ambazo zinatakiwa zikamilishwe meli ikiwa majini.
“Kwa ujumla leo hii nimeridhishwa na kazi inayoendelea hapa kwenye ujenzi huu wa meli hii nimeenda hadi huko uvunguni, kwenye chumba cha kukaa captain mashine zipo na wanaendelea na kazi, watanzania muamini kwamba kazi hapa inaenda vizuri msisitizo ni ule ule kwamba lazima kazi ikamilike kwa asilimia 100 na uzuri hadi hapo walipofikia hawatudai bali sisi ndiyo tunawadai meli," ameeleza.
“Kama alivyoagiza Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwamba kazi iendelee nawahakikishia wananchi na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi mliopo hapa miradi yote itakamilika kwa wakati na mingine itaongezwa tuko kazini muda wote hakuna mradi utakaokwama.
“Nirudie kutoa wito kwa wasaidizi wote wanaomsaidia kazi Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan mawaziri, makatibu wakuu, wakuu wa mikoa , wakurugenzi, wakuu wa wilaya na wengine wote tuchape kazi ili watanzania waone faida ya uwepo wa serikali yao, nirudie tena kuwahakikishia wana CCM hakuna mradi ambao utashindwa kutekelezwa kwa sababu wasaidizi wa Mhe.Rais tumejipanga kuisimamia vizuri,”amesisitiza Mhe. Majaliwa.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Mhandisi Godfrey Kasekenya amesema meli hiyo n kama haitakuwa na changamoto itakabidhiwa kwa wahusika ambao ni Kampuni ya Huduma za Meli Tanzania (MSCL) kwa ajili ya kuanza kuiendesha.
“Sifa za meli hii itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 1200, tani 400 za mizigo, itakuwa na madaraja sita, itaweza kubeba viongozi wakuu wa kitaifa wawili, VIP nne, first class 60, business class 100, second class 200 lakini pia itakuwa na wasafiri wa kawaida kama 834, inaukumbi wenye uwezo wa kubeba watu 400 ambao wanaweza kufanyia sherehe humo kwa hivyo itakuwa ni kivutio kizuri sana na itafanya safari zake katika nchi zote ambazo ziko ukanda wa ziwa viktoria,"amesema Mhe, Kasekenya.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.