Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa Majaliwa ameridhishwa na utekelezaji wa ujenzi wa Daraja la J.P.Magufuli ( Kigongo Busisi ) na kuwahakikishia wananchi kwamba daraja hilo litakamilika kama ilivyopangwa kufikia Februari 2024 kutokana na daraja hilo kufikia asilimia 54 ya utekelezaji wake.
Mhe. Majaliwa amesema hayo mara baada ya kuwasili eneo la Busisi alipokuwa akizungumza na wananchi na kuwaeleza kuwa ameanza Ziara yake kwa kukagua Daraja la J.P. Magufuli (Kigogo - Busisi) lenye urefu wa kilomita 3.2 na barabara unganishi kilomita 1.66,linalosimamiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).
"Miradi yote waliyoianzisha hakuna mradi utakwama, Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mama Samia ambaye alikuwa Makamu wake na mimi pia nilikuwepo na Mama Samia sasa ni Rais kamili na mimi namsaidia Mhe.Rais Samia hakuna kitu kitakwama," amesema Mhe.Majaliwa.
Aidha, Mhe, Majaliwa amewataka wananchi kuendeleza ushirikiano wa kutunza miundombinu na vifaa vinavyotumika katika daraja hilo kwani kwa kufanya hivyo zitatumika fedha zilizopangwa bila kuongeza nyingine.
Akitoa taarifa ya maendeleo ya Mradi huo Mhandisi Paschal Ambrose amesema hadi kukamilika kwake utagharimu shilingi Bilioni 716.333 ikiwa inajumuisha Mkandarasi Shilingi Bilioni 699.278, Mhandisi Mshauri wa usimamizi wa Ujenzi Shilingi Bilioni 11.106, pamoja na fidia Bilioni 3.145 na Usanifu Bilioni 2.803.
Ameongeza kuwa, hadi sasa Mradi umetoa jumla ya ajira 864, kati ya hizo ajira 809 sawa na asilimia 93.63 zimetolewa kwa Watanzania na ajira 55 sawa na asilimia 6.37 ni za wageni na kubainisha kuwa unazingatia Jinsia kwani asilimia 2.31 ya wafanyakazi wote ni wanawake.
"Mradi huu unatumika kama sehemu ya mafunzo kwa kada za Kihandisi, hadi sasa kuna jumla ya Wahandisi 12 wanaopata mafunzo kwa vitendo, kati ya hao 3 wanatoka TANROADS na 9 ni wale waliopita kwenye Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) na yataendelea kuwa endelevu na tunategemea hadi kukamilika kwa Mradi huu Wahandisi wa kutosha watakuwa wamejengewa uwezo na ujuzi kwa ajili ya kusaidia Taifa," amesema Mhandisi Ambrose.
"Daraja hili litakuwa kiungo muhimu kati ya Mikoa ya Mwanza, na Mikoa mingine ya Kanda ya Ziwa pia Nchi za jirani za Rwanda, Burundi,na Uganda na litakuwa kichocheo kikubwa cha kupunguza umaskini na kuhakikisha ukuaji wa uchumi katika eneo la Kanda ya Ziwa na Nchi za Maziwa makuu pamoja na kuondoa msongamano wa magari uliokuwa unatokea kwa wavukaji na kupunguza muda wa kusafiri," ameongeza.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.Adam Malima amesema amefarijika sana na ujio wa ugeni huo kwani ni baraka na faraja kwa wananchi wa Mwanza na kumuomba Mhe.Waziri Mkuu kufikisha salamu za Shukurani za wanamwanza kwa Mhe.Rais.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuleta fedha za miradi ya maendeleo ya kimkakati iliyopo Mkoa huo.
Mradi huu unafadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia 100 na upo chini ya Mkandarasi China Civil Engineering Construction Corporation akishirikiana na China Railway 15 Bureau Group Cooperation (CCECC -CR15GJV zote za China ambapo utekelezaji kwa ujumla umefikia asilimia 54 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Februari 24,2024
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.