Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa amewataka Wananchi kuendelea kuwa na Imani na Serikali ya awamu ya Sita inayosimamia Miradi yote nchini ambayo itakamilika kwa wakati.
Akizungumza Mkoani Mwanza katika ziara yake ya siku moja Mhe Majaliwa amesema licha ya kuwepo changamoto za hapa na pale katika baadhi ya Miradi lakini Serikali imesimama imara kuona Miradi ikikamilika kwa mujibu wa miongozo ya Mikataba.
"Nimefika hapa Mwanza nimekagua ujenzi wa Meli mpya Meli ya MV Mwanza HAPA KAZI sijaridhishwa na mwenendo wa Mkandarasi upo ubabaishaji niwaondoe shaka Wananchi hakuna kitakacho kwamisha kukamilika kwa Mradi"
"Hapa hatoki mtu hadi tunakabidhiwa Meli hii tulimpa muda wa miezi 22 baada ya kutokea changamoto ya Uviko19" amesisitiza Mhe Waziri Mkuu.
Aidha Mhe Majaliwa ameonesha kuridhishwa na Maendeleo ya ujenzi wa Daraja la JP Magufuli lililopo Kigongo Busisi na kuwataka Wafanyakazi kutanguliza uzalendo kwa kuepuka vitendo vya hujuma katika Miradi ya Maendeleo.
Meli ya Mv Mwanza HAPA KAZI TU inafanyiwa ujenzi na Kampuni ya Gas/Entec kutoka Korea kwa gharama ya zaidi ya Shilingi Bilioni 90.
Akiwa Wilayani Sengerema katika kikao na Watumishi wa Halmashauri za Sengerema na Buchosha,Waziri Mkuu Mhe Majaliwa amewakumbusha Watumishi wote nchini kufanya kazi kwa Uaminifu,Uadilifu na Uwajibikaji.
Amewataka kuwa makini na fedha za Serikali zinazoelekezwa katika Miradi mbalimbali yenye lengo la kuwaletea Maendeleo Wananchi.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe Mhandisi Robert Gabriel amemuhakikishia Waziri Mkuu usimamizi imara wa Miradi yote ya Kimkakati na kuzikabili hujuma zote zinazofanywa na baadhi ya Wafanyakazi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.