Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (MB) anatarajiwa kuwasili Mkoani Mwanza Jumamosi ya Oktoba 15, 2022 Majira ya saa 10 jioni kwa ziara ya kikazi.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Adam Kighoma Malima wakati wa Mkutano na Waandishi wa Habari uliofanyika kwenye Ukumbi wa Ofisi ya Mkoa mapema leo alhamisi Oktoba 13, 2022.
Mhe. Malima ametumia wasaa huo kuwakaribisha wananchi wa Mwanza na Mikoa ya jirani kujitokeza kwa wingi kandokando ya barabara na kwenye Miradi atakayoitembelea kumlaki na kumpokea Kiongozi huyo ambaye atakuwepo mkoani humo kwa ziara ya siku nne.
"Nawaomba wakaazi wa Mwanza tuoneshe uzalendo wa dhati, sote tuungane kumpokea Mgeni wetu na tumwoneshe mapenzi ya dhati huku tukiishukuru Serikali kwa kutuletea Maendeleo kama tunavyoona Miradi mbalimbali inaendelea kutekelezwa kwenye maeneo yetu." Mkuu wa Mkoa.
Akizungumzia ratiba ya ziara amesema ,siku ya jumapili ya Oktoba 16, 2022 kuanzia Majira ya saa 2 asubihi Mhe. Majaliwa atakagua Maendeleo ya Ujenzi wa Daraja la Magufuli Kigongo-Busisi pamoja na kusalimia wananchi wa Busisi kabla ya kuelekea wilayani Kwimba ambako atakagua Maendeleo ya Ujenzi wa Mradi wa Reli ya kisasa (SGR).
Malima amefafanua kuwa katika siku hiyohiyo, kuanzia Majira ya saa 7 mchana Mhe. Waziri Mkuu atazindua Jengo la Huduma ya Macho kwenye Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando pamoja na kuzungumza na wananchi kwenye uwanja wa Mahafali hospitalini hapo.
"Siku ya tatu ya ziara ya Mhe. Waziri Mkuu itaanzia Wilayani Ukerewe kwenye visiwa vya Irugwa majira ya saa 3 asubuhi ambako atakagua ujenzi wa Kituo cha Afya na Maendeleo ya Shule ya Sekondari ya Irugwa kabla ya kuelekea kisiwani Gana ambako akiwa huko atakagua maendeleo ya Ujenzi wa Zahanati pamoja na kusalimia wananchi." Amesema Mhe. Malima.
Ameongeza kuwa mara baada ya shughuli za visiwani Mhe. Waziri Mkuu atarejea Mjini Mwanza ambako anatarajiwa kukagua Maendeleo ya Ujenzi wa Stendi ya Mabasi ya Nyegezi kuanzia Majira ya saa 9 alasiri na baadae atawasili bandari ya Mwanza Kusini kwa ajili ya kukagua maendeleo ya Ujenzi wa Meli ya MV Mwanza 'Hapa Kazi Tu'.
Awali amefafanua kuwa Mkandarasi anayejenga Barabara za Mjini Ukerewe kwa kiwango cha Lami Nyepesi kuikamilisha ifikapo Oktoba 15, 2022 kama alivyoagiza alipofanya ziara wilayani humo mwezi uliopita na ametoa wito kwa watumiaji wa Vyombo vya Moto kuziangatia Sheria za Usalama Barabarani ili kuwalinda watumiaji na kujiepusha na ajali.
Vilevile, Mkuu wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza Kamishna Mwandamizi Msaidizi Ramadhani Ng'anzi amesema jeshi hilo pamoja na mambo mengine litahakikisha katika barabara zote zinazoingia Mkoa wa Mwanza hakutakua na Chombo cha Moto kitakachoharibika na kubaki bila kushughulikiwa kwani tabia hiyo imekua ikisababisha ajali na watembea kwa miguu watapewa uangalizi maalumu ili kuwalinda na ajali za Barabarani.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.