Wizara iwalete wataalam kufanyia uchunguzi Nyayo za Mtu wa Kale Butimba, ni Kivutio cha Utalii: RAS Mwanza
Leo Disemba 27, 2023 Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Balandya Elikana amempokea Ofisini kwake Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dastan Kitandula aliyefika kwa utambulisho na kufanya mazungumzo mafupi.
Katika mazungumzo hayo Balandya amesema Mkoa wa Mwanza unaendelea kujivunia, kuvitumia na kutangaza vyema maeneo yote yenye vivutio vya utalii na kuiomba Wizara kuwaleta wataalamu kuona nyayo za mtu wa kale maeneo ya Butimba na kufanya utafiti ili kiwe kivutio kimojawapo cha utalii.
Amesema nyayo hizo zipo kwenye mawe na endapo zitafanyiwa uchunguzi wa kina itakuwa ni miongoni mwa vivutio vingi vya Utalii ndani ya Mkoa wa Mwanza.
"Mhe. Naibu Waziri kwa upande wa uwanja wetu wa ndege ambao utakuwa kichocheo cha kuwaleta watalii wengi, utaanza kufanyiwa ujenzi mwezi Februari mwakani na kukamilika Agosti baada ya Mkoa kuukabidhi kwa mamlaka ya viwanja vya ndege (TAA) ili kukamilisha zoezi hilo", amesema Balandya.
Kwa upande wake Naibu Waziri huyo amebainisha kuwa yupo Mwanza kwa ziara fupi na akiwa hana muda mrefu kwenye Wizara hiyo analazimika kupita kwenye maeneo mbalimbali na akitoka Mwanza ataelekea Tabora.
"Nimefika Mwanza ili niweze kujionea shughuli na changamoto zilizo kwenye Taasisi zetu na kuzipatia ufumbuzi na mengine kuyafikisha ngazi ya juu kuanzia chuo cha wanyama pori Pasiansi na Chuo cha utalii kilichopo eneo la Isamilo," Mhe. Kitandula.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.