ZAIDI YA BILIONI 5 ZAJENGA KITUO CHA UPASHANAJI TAARIFA UKANDA WA ZIWA VICTORIA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amesema nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki hususani zinazopitiwa na ziwa Victoria zinajenga kwa ushirikiano kituo cha upashanaji taarifa kitakachotumika kudhibiti majanga na uokozi ziwani kwa zaidi ya Tshs. Bilioni 5.
Mhe. Mtanda amesema hayo mapema leo Septemba 19, 2024 ofisini kwake wakati akizungumza na Wahe. Wabunge wa kamati ya kudumu ya bunge la Afrika Mashariki ya masuala ya kikanda na utatuzi wa migogoro katika nchi wanachama waliofika mkoani humo kwa ziara ya kikazi.
Mhe. Mtanda amebainisha kuwa Mwanza ni mkoa wa kimkakati na kuna usalama usio na shaka kwani hakuna tukio lolote la kuhatarisha raia wala mali zao na kwamba wananchi wanaendelea kufanya shughuli zao za kujitafutia kipato kwa amani.
"Hatuwezi kuzungumzia uchumi bila kutaja usalama na Mkoa wa Mwanza tuna pato la Trilioni 13 na tunachangia pato la Taifa kwa asilimia 7.2 na tunashika nafasi ya pili tukitanguliwa na mkoa wa Dar es Salaam pekee." Amesema Mhe. Mtanda.
Aidha, amesema Serikali inaendelea kutekeleza miradi lukuki ya kimkakati ndani ya mkoa huo kama daraja la Kigongo-Busisi linalojengwa kwa Tshs. Bilioni 716 na ujenzi umefikia asilimia 95 huku soko la mjini kati linatekelezwa kwa Tshs. Bilioni 23 na limefikia asilimia 90 ya utekelezaji na mingine mingi.
Mkuu wa Msafara huo Mhe. James Milya (MB) kutoka Tanzania amesema bunge hilo litaendelea kulinda rasilimali zilizopo kwenye maziwa kwa kutunga sheria za kiusalama ambazo zinalazimu nchi wanachama kuzifuata bila masharti yoyote.
Aidha, ameushukuru uongozi wa Mkoa wa Mwanza kwa kusimamia rasilimali za maziwa na kulinda usalama na wameahidi katika kufanikisha hilo wataangalia uwezekano wa kuongeza vitendea kazi vya doria kwenye ziwa Victoria hususani boti za uokozi na doria.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.