ZAIDI YA WANANCHI ELFU 3 WAPATA MAJI SAFI NA SALAMA MURUTANGA-UKEREWE
Mwenge wa Uhuru umezindua Upanuzi wa Mradi wa Maji Murutanga (Tanki la Maji Kagunguli) wenye thamani ya zaidi ya Milioni 279 kutoka chanzo cha Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Uviko 19 wilayani Ukerewe ambao umewanufaisha zaidi ya wananchi elfu tatu.
Akizungumza baada ya Uzinduzi huo leo Julai 13, 2023, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2023 Ndugu Abdalla Shaib Kaim amewapongeza Mkuu wa Wilaya, RUWASA na Watendaji wa Ukerewe kwa ujumla kwa Usimamizi mzuri ulioleta matokeo ya mradi bora unaoendana na thamani ya fedha zilizotumika.
"Mwenge wa Uhuru 2023 umekagua Mradi huu kwa kina na itoshe tu kusema ubora umezingatiwa na hakika RUWASA mmeonesha nia ya kumuunga mkono Mhe. Rais kwa kumtua mama ndoo kichwani na kuwaletea huduma bora ya Maji wananchi." Ndugu Kaim.
Naye, Mbunge Viti Maalumu (CCM) Mhe. Furaha Matondo amesema uwepo wa huduma hiyo utasaidia kuwaondoa wananchi wa Kijiji hicho dhidi ya magonjwa ya mlipuko na tumbo kutokana na uwepo wa maji Safi kwenye makazi yao.
Mapema asubuhi Mwenge wa Uhuru ulifika kwenye Mradi wa Ufugaji Samaki ambapo kiongozi wa mbio za Mwenge ametoa rai kwa Halmashauri kuwainua vijana kwa kuwakopesha fedha kupitia fungu la asilimia 10 za mapato ya ndani ili wakuje mitaji yao na kuweza kuwapa urahisi wa kununua malighafi kama chakula na vifaranga.
Akiweka Jiwe la Msingi kwenye Ujenzi wa Kituo cha Afya Murukilima mradi unaotarajiwa kukamilika Mwezi Septemba mwaka huu kwa kupata Miundombinu yenye thamani ya zaidi ya Milioni 500, Ndugu Kaim amewapongeza kwa Usimamizi mzuri wa mradi ambao utawanufaisha zaidi ya wananchi elfu 58 kwa kupata huduma za afya karibu.
Akikagua shamba la matunda kwenye kijiji cha Gillu lililopandwa miche 2992 aina ya Machungwa na maembe, Ndugu Kaim ametoa wito kwa Mkuu wa Wilaya kufuatilia kwa karibu shamba hilo ili kuipa tija Milioni 27.7 iliyowekezwa na kwenye Madarasa 7 yaliyozinduliwa kwenye Sekondari ya Ilangala ameagiza urekebishaji wa dosari zilizobainika.
Zikihitimishwa mbio za Mwenge wa Uhuru wilayani Ukerewe kwa kukimbizwa kwenye miradi sita yenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 1.1, Kikundi cha Vijana Ufundi ni Ajira kilihiyimisha mbio hizo kwa kushauriwa Maafisa husika kuwapa mafunzo vijana na wote wanaowakopesha ili waweze kutumia vizuri mikopo yao.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.