Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe.Hussein Bashe amezitaka taasisi za umma na binafsi ambazo zinajihusisha na masuala ya utafiti na kilimo kuomba eneo la kudumu katika Viwanja vya Maonyesho ya Wakulima (Nanenane- Nyamhongolo) mkoani Mwanza ili kuweka miundombinu yake ya mafunzo ya vitendo kwa wakulima wote.
Amesema kitendo cha taasisi hizo kujitokeza siku za maonyesho pekee hazitoshi kuwaelimisha wakulima na badala yake wanapaswa kuhamia hapo huku akiwataka kuanza harakati kwa kuihusisha wizara ya kilimo ili kusaidia upatikanaji wa maji eneo hilo muda wote kwa ajili ya kilimo.
Kauli hiyo ameitoa wakati akizungumza na viongozi wa Jeshi la Magereza, Taasisi ya Kilimo Tanzania (TARI), Taasisi ya Tanzania Horticultural Association (TAHA) inayojuhusisha na kuendeleza tasnia ya kilimo na wengineo ambapo aliwataka kuwa na ofisi ndogo na maeneo ya kilimo, utafiti na mafunzo kwa wakulima.
“Kitendo chenu ya kuonekana siku za maonyesho hakiwezi kuwasaidia wakulima, hapa mnatakiwa kuwepo muda wote na siyo siku nane kisha mnatoweka na kurudi maofisini, mnatakiwa kuwa na maji ya uhakika na shughuli zenu zifanyike muda wote kama mnahitaji msaada wa wizara toeni taarifa ili tusaidiene.
“Mfano tumeona namna mazao na mbogamboga zilivyostawi katika vitalu vya magareza na Taha, kama wakulima wote wangepata elimu na utalaamu uliotumika sidhani kama tungekuwa hapa tulipo, sasa mkikaa na utalaamu wenu ndiyo maana wakulima wanakimbia sekta hiyo kwa kuhofia kupata hasara.
“Nashukuru kuona magereza wameanza kujenga ofisi zao hapa, naombeni eneo hili litumike kwa kilimo hata viongozi wengine waje kujifunza hapa, kama taasisi zote za utafiti na kilimo bora zingekuwa maeneo ya kilimo bila shaka wakulima ndio watu wa kutolea mfano kwa kipato kikubwa,”alisema.
Meneja Mkuu Uendeshaji wa Taha, Simon Mlay alimweleza Bashe kwamba kutokana na kulima kwa kutumia mbolea , mbegu bora na kufuata utalaam, mazao yao hukomaa ndani ya miezi miwili huku mbogamboga zikichukua siku 30 hadi 45.
Hata alisema wapo tayari kukaa eneo hilo ikiwa watapewa eneo la kujenga ofisi huku akiomba uongozi unaohusika na viwanja hivyo kuweka uzio ili kuzuia mifugo ya wananchi kuingia katika mashamba hayo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Chato, Mtemi Msafiri, alimuomba Bashe kwamba watu wa Mkoa wa Geita wanaomba kufufuliwa kituo cha utafiti cha Bwaga badala ya kutegemea cha Ukiliguru kilichopo Wilaya ya Misungwi mkoani Mwnaza.
Pia alimuomba kuwafikishia maombi yao Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) kuwahi kutoa taarifa za hali ya hewa ili watendaji na wataalamu wa kilimo waweze kufikisha mapema elimu kwa wananchi.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole alisema wameendelea na uhamasishaji wa kilimo cha mazao na malighafi ikiwa lengo ni kufikia uchumi wa kati.Aliongeza kuwa wananchi wa Sengerema na mkoa wa Mwanza wamehamasika kulima zao la pamba kutokana na jitihada zinazochukuliwa na Serikali.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya maonyesho ya Nanenane yanayohusisha Mikoa ya Mwanza, Kagera na Geita alisema kulikuwa na washiriki 260, halmashauri 12 kati ya 22, wadau wa sekta ya kilimo 150 walikuwa wamehudhuria huku matarajio ni kuwa na wadau 350 walio rasmi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.