Leo Septemba 08, 2025 Kaimu Katibu Mkuu OR- UTUMISHI ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali watu wa wizara hiyo Bw. Musa Magufuli amefungua Kikao cha Kamati ya Kitaifa, Waratibu wa Wizara wa VVU, UKIMWI na Magonjwa sugu yasiyoambukiza mahali pa kazi na wajumbe wa ngazi ya Taifa na Mkoa jijini Mwanza na kutoa maagizo kadhaa.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa wizara hiyo kwenye Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Bw. Magufuli amesema Wizara zina wajibu wa kusimamia ofisi za chini kutekeleza muongozo wa kuthibiti VVU, UKIMWI na Magonjwa sugu yasiyoambukiza mahala pa kazi katika utumishi wa umma (2024) pamoja na Sekretatieti za Mikoa kusimamia LGA's kutekeleza waraka namba 02.
Aidha, amesema katika kufanikisha hayo ni lazima ofisi zitoe mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi pamoja na kuteua na kubuisha kamati na kuteua waratibu na kuwapa vitendea kazi vya kutekeleza afua hizo huku akibainisha umuhimu wa kuhuisha takwimu na kuziwasilisha OR- UTUMISHI pamoja na kutenga bajeti ya kufanikisha.
Awali, amebainisha kuwa kwa mwaka 2025 jumla ya watumishi 1983 wamejiweka wazi kuishi na VVU na UKIMWI kutoka katika taasisi 240 ambapo 884 ni wanaume na 1099 ni wanawake na kwamba kwa kipindi cha julai 2023- Juni 2025 watumishi 18842 wamepatiwa matibabu ya Afya ya Akili katika hospitali ya Taifa Milembe wakiwemo watumishi wa umma jambo linalodhoofisha ufanisi wa utendaji kazi.
Naye, Katibu Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Bw. Balandya Elikana amebainisha juhudi za Mkoa huo katika kukabiliana na VVU, UKIMWI na Magonjwa yasiyo ambukiza kwamba Mkoa huo umeunda kamati za kusimamia utekelezaji wa afua hizo kuanzia ngazi za kata hadi wilaya na kwamba kamati hizo zipo hai pamoja na changamoto ya bajeti finyu.
"Mtu anapokua na mgonjwa mwenye maambukizi ya UKIMWI unakosa muda wa kuzalisha mali kwa kujikita kwenye kumuuguza hivyo Mwanza tunaendelea kutoa Elimu kwa jamii kuachana na tabia hatarishi ili wananchi wawe na afya njema na kuweza kujihusisha na shughuli za usalishaji kama kilimo, uvuvi na ufugaji." Amesema Balandya.
Aidha, amempongeza Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Jesca Lebba kwa kusimamia mazoezi ya watumishi yanayofanyika mara tatu kwa juma na kwa kuongoza mbio na matembezi ya Kilomita tano kila mwezi ikiwa ni juhudi za Mkoa huo katika kuweka afya za watumishi imara na kuepuka magonjwa yasiyo ambukiza.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.